Galatians 6

1Ndugu, ikiwa mtu amekamatwa katika uovu, ninyi mlio wa kiroho, mnawiwa kumrejesha huyo ndugu katika roho ya upole. Huku mkijiangalia wenyewe ili msijaribiwe. 2Mchukuliane mizigo, na kwa hiyo mtaikamilisha sheria ya Kristo.

3Ikiwa mtu yeyote anajiona ni bora wakati si kitu, anajidanganya mwenyewe. 4Kila mmoja na aipime kazi yake. Kisha atakuwa na kitu mwenyewe peke yake cha kujisifu, bila kujilinganisha mwenyewe na mtu yeyote. 5Maana kila mtu atachukua mzigo wake mwenyewe.

6Mtu aliyefundishwa neno lazima amshirikishe mazuri yote mwalimu wake. 7Msidanganyike. Mungu hadhihakiwi. Kila apandacho mtu, ndicho atakachovuna pia. 8Kila apandaye mbegu katika asili yake ya dhambi atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye mbegu katika Roho, atavuna uzima wa milele kutoka kwa Roho.

9Tusichoke katika kutenda mema, maana kwa wakati wake tutavuna ikiwa hatutakata tamaa. 10Hivyo basi, wakati tutakapokuwa na nafasi, tutende mema kwa kila mmoja. Tutende mema zaidi hasa kwa walio ndani ya imani.

11Angalieni ukubwa wa barua nilizowaandikia kwa mkono wangu mwenyewe. 12Wale wanaotaka kufanya mema kwa mtazamo wa mwili ndiyo wenye kuwalazimisha mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu wasiingie kwenye mateso ya msalaba wa Kristo. 13Maana hata hao waliotahiriwa wenyewe hawaishiki sheria. Badala yake wanataka ninyi mtahiriwe ili waweze kujivunia miili yenu.

14Isitokee nikajivuna isipokuwa kwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni katika yeye ulimwengu umesulubiwa kwangu na mimi katika ulimwengu. 15Kwa kuwa haijalishi kutahiriwa au kutokutahiriwa kuwa ni kitu. Badala yake uzao mpya ni muhimu. 16Kwa wote wenye kuishi kwa kanuni hii, wawe na amani na rehema iwe juu yao wote, na juu ya Israel ya Mungu.

17Tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, maana nimebeba chapa za Yesu mwilini mwangu. 18Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe na roho zenu, ndugu. Amina.

Copyright information for SwaULB